Uongozi wa Klabu ya soka ya Yanga umemtimua kazi kuanzia leo tarehe 27 Julai 2020, Kocha Mkuu wa Klabu hiyo Luc Eymael kufuatia kauli zisizo za kiungwana na za kibaguzi alizozitoa kisha kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vingine mbalimbali vya habari.
Kuafuatia kufukuzwa ajira hiyo kwa kocha, Klabu ya Yanga pia imewaambia wanachama, wapenzi na mashabiki wa Klabu hiyo kuwa watahakikisha kocha huyo anaondoka nchini haraka iwezekanavyo.
Katika taarifa ya Yanga iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Wakili Simon Patric, uongozi umewaomba radhi wanachama na wapenzi wote wa soka, viongozi wa nchi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na kauli za kuudhi na kudhalilisha zilizotolewa na Kocha Luc Eymael.
Yanga imeendelea kudai inathamini na kuamini katika misingi ya nidhamu na utu, na inapingana aina yoyote ya Ubaguzi.
Kwa upande wa TFF, Shirika hilo la mpira wa miguu Tanzania, litamchukulia hatua ya kinidhamu Kocha huyo wa Yanga Luc Eymael kwa kumfikisha katika vyombo husika kutokana na matamshi ya kibaguzi aliyoyatoa kwa washabiki wa timu hiyo.
Vilevile TFF itawasilisha taarifa za Eymael kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuhusu kauli hizo ili nalo lichukue hatua, kwani kocha huyo bado anaweza kufanya vitendo hivyo katika nchi nyingine.
Kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Katiba ya FIFA, vitendo vya kibaguzi vya aina yoyote ile haviruhusiwi katika mpira wa miguu.