Wine, mwanamuziki maarufu aliyegeuka kuwa mwanasiasa aliyeshindana na Rais mkongwe Yoweri Museveni katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2021 nchini Uganda, amekuwa akikamatwa mara nyingi.
Katika nchi jirani ya DR Congo, kiongozi wa upinzani Moise Katumbi amewasilisha ombi lake la kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Desemba ambapo Rais Felix Tshisekedi anawania tena nafasi hiyo kwa muhula wa pili, chama chake kilisema siku ya Jumatano. Katumbi, mfanyabiashara tajiri mkubwa na gavana wa zamani wa mkoa wa Katanga wenye utajiri wa shaba, pia atashindana dhidi ya Martin Fayulu - ambaye aliibuka mshindi wa pili katika uchaguzi uliopita - na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya magonjwa ya wanawake Denis Mukwege na wengineo.
Nako nchini Burundi, mahakama nchini Burundi imemnyima dhamana waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Alain-Guillaume Bunyoni, ambaye ameshtakiwa kwa shutuma za kuhujumu usalama wa taifa na kumtusi rais, vyanzo karibu na kesi hiyo viliambia vyombo vya habari siku ya Alhamisi. Bunyoni alikuwa waziri mkuu kuanzia katikati ya mwaka 2020 lakini aliachishwa kazi kutokana na mzozo wa ngazi ya juu wa kisiasa mwezi Septemba mwaka 2022, siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuonya kuhusu njama ya "mapinduzi" dhidi yake. Mkuu huyo wa zamani wa polisi na waziri wa usalama wa ndani, Bunyoni alikuwa akionekana kama mkuu wa baraza la viongozi la kijeshi linalojulikana kama "majenerali" wenye nguvu ya kweli ya kisiasa nchini Burundi.
Na baada ya wiki kadhaa za uvumi, hatimae Rais wa Kenya William Ruto Jumatano alifanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri, kuongeza wizara mpya, na kuwateua maafisa wapya kuchukua nyadhifa mbalimbali serikalini. Mawaziri 8 ni kati ya waliohamishiwa kwa wizara nyingine huku majukumu ya Waziri Mkuu Musalia Mudavadi yakiongezwa, na idara moja kuondolewa kutoka kwa afisi yake. Rais Ruto pia aliwateua makatibu wakuu kadhaa, mabalozi na manaibu wao, huku akiwahamisha wengine kuhudumu katika wizara au balozi mbalimbali. Rais huyo alifanyia mabadiliko baadhi ya wizara, huku idara mbalimbali zikihamishwa.