Mabalozi wengi kwenye Umoja wa Mataifa wameunga mkono pendekezo linaloishinikiza Urusi kusitisha mashambulizi yake nchini Ukraine. Hatua hiyo ilifikiwa katika kikao cha dharura na cha nadra cha Baraza Kuu la Umoja huo.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameelezea kutoridhishwa kwake na matukio yaliyoripotiwa ya unyanyasaji wa baadhi ya raia wa Nigeria wanaojaribu kuondoka Ukraine baada ya Russia kuivamia nchi hiyo. Wanigeria 4,000 bado wamekwama Ukraine. Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Twitter ofisi ya rais imesema maafisa wa polisi na usalama wa Ukraine wameripotiwa kuwakatalia wanigeria kupanda mabasi na treni kuelekea kwenye mpaka wa Ukraine na Poland. Ofisi ya Buhari imesema raia wote wa kigeni wanaojaribu kuvuka mpaka wa Poland lazima wahudumiwe kwa kufuata utu na bila upendeleo.
Wanamgambo wa Kiislamu wanatuhumiwa kuua takriban raia 20 kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo majira ya usiku. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa raia wa ndani na mwanaharakati ambaye amekosoa kushindwa kwa vikosi vya Congo na Uganda kuzuia mauaji hayo. Shambulizi la Jumapili jioni katika kijiji cha Kikura lililaumiwa na mkazi na mwanaharakati wa ADF, mwanamgambo wa Uganda ambaye ameuwa maelfu ya raia mashariki mwa Congo tangu mwaka 2013.