Kiongozi wa Upinzani wa Victoria Matthew Guy amesema matokeo ya kura za maoni za chama chake yanaonesha chama cha mseto kinaweza wania uongozi katika uchaguzi mkuu ujao wa Victoria, licha ya tafiti kudokeza ushindi mwingine wa chama cha Labor.
Wakaaji katika maeneo yanayo athiriwa na mafuriko jimboni NSW, wana hamasishwa waendelea kuwa waangalifu dhoruba nyingine ikitarajiwa kugonga sehemu za jimbo hilo wiki hii. Amri kadhaa zakuondoka zilitolewa jana katika kanda nzima ya Hawkesbury, na sehemu za kati magharibi na kanda ya Riverina ya jimbo hilo.
Wizara ya afya ya Malawi inasema hivi karibuni itatoa chanjo ya kwanza ya malaria barani Afrika kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Chanjo ya RTS,S, ambayo ilijaribiwa nchini Ghana, Kenya, na Malawi, ilichukua zaidi ya miaka 30 kutengenezwa. Utoaji wa chanjo, uliopangwa kufanyika mwezi ujao, unafuatia kukamilika kwa awamu ya majaribio. Tangu mwaka 2019, Shirika la Afya Ulimwenguni limechanja watoto 360,000 kwa mwaka nchini Malawi, Ghana na Kenya, na theluthi moja yao nchini Malawi.