Wasafiri katika uwanja wa ndege wa Sydney wame hamasishwa waruhusu muda wa ziada, kusimamia uhaba wa wafanyakazi unao sababisha usumbufu wa usafiri wakati wa likizo za shule. Wasafiri wanashauriwa wawasili masaa mawili kabla ya safari zao kwa sababu ya matatizo ya sekta ya usafiri wa ndege, yanayo endelea katika viwanja kadhaa vya ndege.
Zaidi ya watu 30 waliuawa katika mashambulizi yaliyotekelezwa Jumapili na Jumatatu na washambuliaji wanaoshukiwa kuwa wanajihadi katika mkoa wa kaskazini mashariki mwa DRC wa Ituri, shirika la mslaba mwekundu limesema. Waasi wa ADF walishambulia raia katika vijiji viwili karibu na Komanda, umbali wa kilomita 75 na mji wa Bunia, amesema David Beiza, mkuu wa shirika la mslaba mwekundu katika wilaya ya Irumu mkoani Ituri. Kundi linalofuatilia masuala ya usalama DRC, Kivu Security Tracker ( KST), liliripoti baadaye kwenye Twitter kwamba watu 18 waliuawa Jumatatu katika kijiji cha Mangusu, na kuongeza kuwa ADF wanashukiwa kutekeleza mauaji hayo.
Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kufanya mazungumzo mjini Vienna na wawakilishi wa jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani, OPEC, leo Jumatatu, kukiwa na wito wa kuitaka jumuiya hiyo wa kuongeza uzalishaji wa mafuta. Jumuiya ya OPEC imekataa miito ya Marekani na wakala wa nishati wa kimataifa kuongeza uzalishaji wa mafuta ghafi ili kupunguza bei ya mafuta duniani iliyofikia kilele mwezi uliopita katika muda wa miaka 14 baada ya Marekani na Umoja wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine. Jumuiya ya OPEC inayojumuisha pia Urusi, itaongeza uzalishaji wa mafuta kwa takriban mapipa 432,000 kwa siku kuanzia mwezi ujao wa Mei.