Queensland imetangaza mpango mpya wenye lengo lakutoa msaada, kwa afya ya akili ya vijana kote jimboni. Waziri wa afya Yvette D'Ath amesema $8 milioni zitatumiwa mtandaoni, kutoa tiba na zana katika jaribio la miaka mbili, kwa lengo lakuwasaidia vijana wanao omba huduma katika baadhi ya hospitali za umma za Queensland, pamoja na shirika la HeadSpace.
Marekani imepokea taarifa za kipelelezi kuwa uvamizi wa Urusi, dhidi ya Ukraine unaweza kutokea mapema Jumatano. Ubalozi wa Marekani mjini Kyiv umeanza kuwaondoa wafanyakazi wake. Kwa kuongezea, Wizara ya Mambo ya Nje imetoa tahadhari ya kusafiri ikionya watu kutokwenda Ukraine “ kutokana na kuongezeka kwa vitisho vya hatua za kijeshi za Russia” na kuwashauri “ wale wote walioko Ukraine kuondoka mara moja.”
Viongozi kutoka Kongo zote mbili, Uganda na Togo walikutana hapo jana Jumamosi kujadili usalama katika eneo la Afrika ya kati na mapinduzi ya hivi karibuni huko magharibi mwa bara hilo. Taarifa rasmi imeeleza kwamba marais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Denis Sassou Nguesso wa Kongo-Brazzaville na Yoweri Museveni wa Uganda aliyewakilisha maeneo ya maziwa makuu pamoja na Faure Gnassingbe wa Togo kutoka Afrika Magharibi, walikutana karibu na mji mkuu wa Congo Brazzaville.