Maafisa wa afya wa Queensland wamesema shinikizo dhidi ya mfumo wa hospitali za jimbo hilo, inaanza kupungua. Jimbo hilo limepata sehemu ya mwisho ambako ujenzi wa hospitali saba, utafanywa kuanzia baadae mwaka huu. Hali hiyo imejiri wakati jimbo la Queensland, limerekodi kifo cha sita cha UVIKO-19 pamoja na kesi mpya 3,750 za maambukizi.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amemhimiza Rais wa Urusi Vladimir Putin kurudi nyuma kutoka eneo hatari la kukaribia kutumbukia vitani, huku akitahadharisha kwamba uvamizi wa Ukraine unaweza kufanyika katika kipindi cha saa 48 zijazo. Johnson ameieleza hali katika mpaka wa Ukraine kuwa ngumu na ya hatari kubwa huku akiwataka washirika wa Magharibi kusimama pamoja kuonesha mshikamano na nchi hiyo.
Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan Jenerali Abdel Fattah Burhan amekutana na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat mjini Khartoum Jumapili kujadili masuala ya kisiasa nchini Sudan. Mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wa Sudan, Dr al-Rasheed Ibrahim amesema makubaliano yoyote au juhudi zitasaidia mkakati wa uthabiti wa Afrika. Faki pia atakutana na vyama vya upinzani kusikiliza na kujadiliana nao kuhusu mtazamo wao katika ziara yake ya siku mbili nchini humo.