Waziri Mkuu mteule amesema mkutano wa Quad wiki hii, utakuwa fursa ya kwanza ya chama cha Labor kujumuika katika hali tofauti na mataifa mengine kwa mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na maswala mengine. Mkutano wa QUAD utafanyika mjini Tokyo tarehe 24 Mei kati ya viongozi wa mataifa ya Japan, Australia, India na Marekani.
Wakati huo huo waziri mkuu anayeondoka madarakani Scott Morrison, amezungumza mbele ya waumini wenza katika kanisa lake katika moja ya hotuba zake za mwisho kama waziri mkuu wa Australia. Alipozungumza ndani ya kanisa lakipentekosti la Horizon mjini Sydney, Bw Morrison alinukuu maandishi matakatifu nakuzungumza kuhusu kupoteza uchaguzi mkuu kwa chama cha Labor, ambacho kwa sasa ina aminika kimeshinda viti 77 wakati mseto wa Liberal na Nationals wameshinda viti 54.
Chama cha Communist cha Sudan kimesema kwamba serikali mapema Ijumaa imeachilia huru wapinzani wawili wa mapinduzi ya kijeshi siku moja baada ya kukamatwa. Mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba mwaka jana nchini humo yamezua maandamano ya kitaifa na kupelekea msako mkali uliosababisha vifo vya takriban watu 95 huku mamia wengine wakijeruhiwa kulingana na ripoti kutoka muungano wa madaktari.