Viongozi wa nchi zenye nguvu kiuchumi duniani wanafanya mkutano kwa njia ya video kujadili namna ya kupambana na corona na kuufufua uchumi wa ulimwengu. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewahimiza viongozi wa nchi za G20 kuendelea kushirikiana katika vita dhidi ya virusi vya corona, akiuambia mkutano wa kilele unaofanyika kwa njia ya video kuwa mengi yanastahili kufanywa ili kulidhibiti janga hilo.
Mgombea urais wa Uganda na muimbaji mashuhuri Bobi Wine ameachiliwa kwa dhamani ijumaa wakati vifo vimefikia 37 vilivyo sababishwa na maandamano makubwa nchini humo. Mwanasiasa huyo ameachiliwa baada ya maafisa wa usalama kumfungulia mashtaka kwa madai ya kuwa kitendo chake cha kampeni kingeliweza kusambaza virusi vya corona.
Serikali ya Ethiopia imekataa juhudi za Umoja wa Afrika za upatanisho na kusema wanajeshi wake wamechukua udhibiti wa mji mwengine wakati jeshi la serikali linapoelekea katika mji mkuu wa mkoa wa kaskazini wa Tigray unaoshikiliwa na waasi. Mnamo siku ya Ijumaa, Umoja wa Afrika uliwateua marais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano, Ellen Johnsof Sirleaf wa Liberia na Kgalema Motlanthe wa Afrika Kusini kama wajumbe maalum katika mazungumzo ya upatanisho.