Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres asikitishwa na ukosefu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia hi leo, alipokuwa anafungua mkutano wa viongozi kuadhimisha miaka 75 tangu kuundwa kwa umoja huo.
Jaji mkuu nchini Kenya David Maraga amemtaka rais Uhuru Kenyatta kulivunja bunge kwasababu halina wabunge wanawake wa kutosha. Katiba inasema kwamba jinsia moja haiwezi kudhibiti zaidi ya thuluthi mbili ya viti vya bunge. Hatahivyo wanawake wana viti vichache ikilinganishwa na viti 116 vinavyohitajika katika bunge hilo la wabunge 350.
Mali imewatangaza viongozi wa serikali mpya ya mpito, ambao utaweza kuendeleza mahusiano madhubuti na jeshi pamoja na uwepo wa shinikizo la kimataifa la kuteuliwa kwa kiongozi raia baada ya mapinduzi ya kijeshi. Katika taarifa yake ilioneshwa kwa njia ya video, kiongozi wa kijeshi Kanali, Assimi Goita amesema waziri wa zamani wa ulinzi Bah Ndaw, atakuwa rais wa serikali ya mpito wakati yeye mwenyewe atahudumu kama makamo wa rais.