Sehemu za kaskazini New South Wales zinakabiliana na mafuriko makubwa baada ya mvua nyingi na dhoruba, wakati ofisi ya utabiri wa hewa imetangaza kutakuwa mvua nyingi zaidi hadi mwisho wa mwaka. Na Tasmania inazingatia kuchelewesha mwanzo wa shule wa mwaka wa 2022, kwa ajili yakuwapa wanafunzi fursa yakuchanjwa dhidi ya UVIKO-19.
Uganda inasema kwamba washukiwa saba wameuwawa na wengine 106 wanashikiliwa kutokana na matukio ya kigaidi. Hayo yametokea wakati wa oparesheni iliyofanywa na vikosi vya usalama wakihusishwa na washukiwa watatu wa mabomu ya kujitoa muhanga katika mji mkuu Kampala wiki iliyopita, kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Reuters ya Jumatatu.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema yuko tayari kuelekea kwenye uwanja wa mapambano kuongoza wanajeshi wa serikali wanaopambana na wapiganaji waasi. Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Twitter, Waziri Mkuu Abiy Ahmed ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2019 amesema yuko tayari kuwa katika mstari wa mbele kuongoza mapambano dhidi ya waasi. Ameandika, "Wale wanaotaka kuwa miongoni mwa watoto wa Ethiopia ambao watasifiwa na historia, amkeni kwa ajili ya kuitetea nchi yenu leo. Tukutane katika mstari wa mbele."