Mashirika ya upangaji yamesema wapangaji katika maeneo ya kaskazini NSW yaliyo athiriwa na mafuriko, wanakabiliwa na ongezeko ya magumu katika miezi ijayo, wakati mchakato wa uponaji unaendelea. Na kiongozi wa Queensland, Annastacia Palaszczuk ametangaza kuwa amri za chanjo zita isha Alhamisi wiki ijayo, mida ya saa saba usiku wa 14 Aprili kwa sehemu nyingi za matukio jimboni humo.
Raia mmoja wa Rwanda aliyeorodheshwa kama shujaa katika filamu ya Hotel Rwanda, hapaswi kuongezewa kifungo chake cha miaka 25 hadi kifungo cha maisha jela mahakama ya Rwanda iliamua Jumatatu. Paul Rusesabagina alipatikana na hatia mwezi Septemba kwa mashtaka manane ya ugaidi kwa jukumu lake katika kundi moja linalompinga Rais Paul kagame. Alisema kwamba yeye alikuwa kiongozi wa chama cha Rwanda Movement for Democratic Change lakini hakuwa na jukumu lolote katika mrengo wa kijeshi wa kundi hilo la National Liberation Front ambalo limefanya mashambulizi. Familia yake inafanya kampeni ya kuomba kuachiliwa kwake, ikisema Rusesabagina ni mgonjwa. Rusesabagina aliwaokoa takribani watu 1,200 kwa kuwahifadhi katika hoteli wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambapo zaidi ya watu laki nane waliuawa.
Hasira na lawama kutoka nchi za magharibi zimeendelea kuiandama Urusi kuhusiana na mauaji ya watu wengi ambao nchi hizo zinavishutumu vikosi vya Urusi kuyafanya katika mji wa Ukraine wa Bucha. Ujerumani pekee imesema itawafukuza wanadiplomasia wa Urusi wapatao 40, Ufaransa itawarudisha nyumbani wapatao 35, na Lithuania imesema itawatimua wanadiplomasia wa Urusi ambao bado haijataja idadi yao. Urusi imesema itazijibu nchi hizo kwa hatua sawa na hizo. Katika hatua nyingine inayozidisha utengano baina ya Urusi na nchi za magharibi, hapo jana rais wa Urusi Vladimir Putin alitia saini amri inayofuta urahisishaji wa viza za nchi yake kwa maafisa na waandishi wa nchi za Ulaya alizoziita mahasimu.