Victoria ime rekodi maambukizi mapya 980 ya UVIKO-19, pamoja na vifo saba. Hali hiyo imejiri wakati serikali imesema itatumia dola milioni 113, kuwasaidia watoto kushiriki katika shughuli walizo penda kabla ya janga la UVIKO-19. Watoto wataweza furahia kushiriki katika kambi, miradi ya michezo pamoja na shughuli zingine zakitamaduni katika mwaka wa 2022, kama sehemu ya mpango wa jimbo hilo kufunguliwa tena.
Wizara ya Elimu ya Ethiopia imetangaza kufungwa kwa shule zote za sekondari kwa muda mfupi, ili kuwaruhusu wanafunzi kusaidia katika kuvuna chakula katika mashamba ya Waethiopia wanaopigana vita dhidi ya kundi la wapiganaji wa TPLF. Shirika la habari lenye uhusiano na serikali ya Ethiopia, FANA, limeripoti kwamba waziri wa elimu Berhanu Nega amesema kwamba shule zitafungwa kwa muda wa wiki moja. Serikali ilisema Jumatatu kwamba zaidi ya wanafunzi milioni 1.2 hawapo shule kutokana na mapigano yanayoendelea kaskazini mwa nchi hiyo. Mapigano yameharibu mamia ya shule.
Watu wasiopungua 20 wa kwaya ya Kanisa Katoliki la Mwingi wamefariki baada ya basi walilokuwa wanasafiria kutumbukia katika Mto Enziu, kaunti ya Kitui, kusini mashariki mwa Kenya, Jumamosi. Hadi sasa, miili 20 imepatikana kutoka katika basi na watu wengine 10 wameokolewa na kupelekwa katika Hospitali ya Mwingi Level Four kwa matibabu ya dharura. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kitui Leah Kithei, basi hilo yenye siti 51 linalomilikiwa na Mwingi Junior Seminari, Shule binafsi inayoendeshwa na Kanisa Katoliki, ilikuwa inawasafirisha wana kwaya kwenda eneo la Nuu kutoka mji wa Mwingi kuhudhuria sherehe za harusi.