Kiongozi wa New South Wales Chris Minns amesema kipaumbele cha serikali yake niku kabiliana na mgogoro wa makazi kwa kupiga jeki utoaji wa sera rafiki za maendeleo. Kauli hiyo imejiri baada ya jengo katika eneo la Kaskazini Strathfield, ambalo liko katika maeneo ya ndani ya magharibi Sydney, limekuwa lakwanza kutoa makaazi kwa kutumia bonasi ya makazi ya bei nafuu ya serikali ya Minns.
Wauguzi jimboni Queensland wanatihsia kufanya mgomo baada ya chama cha wauguzi jimboni humo, kutoa hati ya mwisho ya mpango wa malipo kwa serikali ya jimbo hilo. Sarah Beaman ni katibu wa chama hicho, amesema waziri wa afya wa jimbo hilo yuko na hadi Jumanne kukubali masharti ya chama cha wauguzi la sivyo, wata chukua hatua ya pili ya mgomo huo mwanzoni mwa Julai.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema makubaliano ya amani kati ya nchi yake na Rwanda yana lengo la kumaliza miongo kadhaa ya ghasia mashariki mwa DRC na yanafungua njia ya kuanza kwa "zama mpya ya utulivu". Felix Tshisekedi ameitoa kauli hiyo leo wakati nchi yake ikiadhimisha miaka 65 tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa wakoloni Ubelgiji , kumbukumbu ambayo inafanyika wakati huu kukishuhudiwa mizozo katika eneo la mashariki mwa Kongo.
Boniface Kariuki, mchuuzi aliyepigwa risasi kichwani wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi Juni 17, 2025 ameaga dunia, familia sasa yathibitisha. Msemaji wa familia Emily Wanjira alisema kupitia mawasiliano ya simu kwamba Boniface alikata roho leo (Juni 30, 2025) 3.15pm baada ya kuwa mahututi tangu alipokimbizwa hospitalini na Wasamaria Wema baada ya kupigwa risasi kichwani na polisi wakati wa maandamano ya Juni 17, 2025.