Kundi la wazima moto wa Australia, wana elekea nchini Canada kuwasaidia washirika wao ambao wanakabiliana na moto wa nyika jimboni Alberta. Maafisa hao wanatumwa chini ya masharti ya mkataba wa makubaliano yaliyo anzishwa kati ya nchi hizi mbili, zinazo husiana na ushirikiano ambao unaweza hitajika katika matukio ya dharura.
Mgogoro kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda umechukua sura mpya kufuatia uamuzi wa Rwanda kujitoa katika Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati (ECCAS). Rwanda inadai kuwa DRC ilishirikiana na baadhi ya nchi wanachama wa ECCAS kuizuia kuchukua nafasi ya uenyekiti wa jumuiya hiyo.
Idara ya Polisi nchini Kenya inamulikwa kwa kifo cha kutatanisha cha Mwalimu Albert Ojwang', aliyekuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii. Ojwang' alifia kwenye korokoro ya kituo kikuu cha polisi jijini Nairobi baada ya kukamatwa kwao katika jimbo la Homa bay kwa madai ya kuchapisha taarifa za uwongo kwenye mtandao wa X.