Jamii ya Sudan walio Australia waendelea kuwa na wasiwasi

South Sudanese Australian

A South Sudanese Australian voter in the referendum Credit: Ajak Chiengkou

Jamii ya watu wa Sudan walio nchini Australia wana wasiwasi mkubwa ,wakisubiri habari kutoka kwa familia zao walionaswa katika jiji la Al-Fasher baada ya mlipuko wa ghasia. Jiji hilo lilitekwa na Rapid Support Forces wiki mbili iliyopita, na wataalamu wanaamini kwamba maelfu huenda wameuawa katika mauaji ya kutisha. Kwa kuwa huduma za intaneti na simu zimekatwa, wanaoishi nje ya nchi wanalazimika kukaa na kusubiri ili kujua kama wapendwa wao bado wako hai.


"Binafsi nahisi kufa ganzi Tangu kuchukuliwa madaraka. Siku tatu za kwanza nimekuwa na mlo mmoja. Siwezi kula, siwezi kufikiria jambo lingine lolote. Ami yangu, hatujui kama ameaga au yuko hai
Abdelrasul
"Kumekuwa na ukosefu kamili wa mawasiliano. Sijasikia kitu chochote kutoka kwa familia au marafiki walioko huko. Imeathiri sana afya yangu ya akili, si mimi pekee, wengi wa wasudani imeathiri afya zetu za akili sana na hata hatuko huko. Tunatazama tu video
Mohammed
 Algaly Abdelrasoul na Duha Mohammed ni WaSudan-Waustralia ambao wamejawa na hofu kuwa huenda wanafamilia wao walioko Sudan wameuawa. Wapenzi wao wamekwama katika jiji la Al-Fasher, mji mkuu wa eneo la magharibi la Sudan, Kaskazini mwa Darfur.

Baada ya kunusurika kwenye mzingiro wa njaa wa miezi 18 wa jiji hilo na kundi la kijeshi la Rapid Support Forces, au RSF, sasa wamejikuta katika hatari baada ya wanamgambo kuvamia Al-Fasher wiki mbili zilizopita , na inaripotiwa walifanya mauaji makubwa ya raia.

Alkheir Ismail alikimbilia mji wa karibu wa Tawila, akisema alifanikiwa kutoroka mojawapo ya maeneo ya mauaji.

 
Watu hawa walitukusanya sisi raia 300, wasafiri, walituletea kwenye bwawa. Watu walio kwenye ngamia na pikipiki walitukusanya na kutuua hapo. Hii ilikuwa Jumapili. Baada ya hapo, kulikuwa na kijana mmoja niliyesomana naye, katika chuo kikuu huko Khartoum, aliwaambia, 'msimuue.' Baada ya hapo waliwaua watu waliobaki, vijana pamoja nami na marafiki zangu.
Alkheir Ismail


Nathaniel Raymond ni mchunguzi wa uhalifu wa kivita, na Mkurugenzi Mtendaji wa Maabara ya Utafiti wa Kibinadamu ya Yale, ambayo imekuwa ikichambua ushahidi wa setilaiti wa madai ya uhalifu huko Al-Fasher.

Anasema kiwango cha umwagaji damu ni cha kushangaza.
 
Kile ambacho tunaweza kuwaambia ni kwamba hatuzungumzii mamia, hatuzungumzii chini ya 10,000. Sasa tunahamia kwenye makumi ya maelfu. Ili kuweka hili katika mtazamo, tunakabiliwa na mauaji ya kiwango cha Rwanda, na dunia kwa sasa inapaswa kulenga kwa umakini kinachoendelea Al-Fasher. Madhara ya kinachotokea pale yanaweza kuwa hayako dhahiri (bado) lakini yatakuwa
Nathaniel Raymond


Serikali ya Sudan inasema kuwa angalau raia 2,000 waliuawa katika saa 48 za mwanzo za kuchukuliwa kwa mamlaka na R-S-F, huku Shirika la Afya Duniani pia likiripoti kwamba watu 460, wakiwemo wagonjwa na wafanyakazi wa matibabu, waliuawa katika hospitali ya uzazi ya Saudi ya mji huo.

R-S-F imekuwa ikipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe na jeshi la Sudan tangu Aprili 2023 lakini kukamatwa kwa Al-Fasher ni maendeleo makubwa. Kwa vile mji sasa umeangukia kwa kundi la wanamgambo, kundi hilo lina udhibiti kamili wa maeneo ya Darfur ambayo yana ukubwa wa theluthi moja ya nchi.

Tangu kuchukuliwa kwa mamlaka, huduma za simu na upatikanaji wa intaneti zimekatwa kote mjini, wakiwatenganisha na wale wanaoishi nje ya nchi.

Duha Mohammed alitoroka vita na anaishi Canberra. Familia yake inalazimika kutafuta video za mauaji zilizowekwa na wanamgambo wakijisifia mashambulizi kwenye mji wao.

Tumekuwa tukitazama video ambazo zinaibuka, tukijaribu kuona kama tutakutana na sura TUNAYOFAHAMU miongoni mwao, kama tutamwona jamaa, rafiki, au mwanafamilia, kama tutaweza kumtambua yeyote kati yao. Kila tunapopitia video na sikumbuki mtu yeyote ninayemfahamu, ninapata hisia za afueni kwamba niko sawa, inamaana hawakuwa sehemu ya watu walioteswa. Lakini wakati huo huo, ninajiuliza, 'wako wapi?' Hii haimaanishi kwamba wako salama
Duha Mohammed
 

Mjomba wa Algaly Abdelrasoul, shangazi na familia ya mbali wamekwama huko Al-Fasher. Anasema amezoea kupoteza wapendwa kutokana na vita vya miaka miwili na nusu, lakini kilicho kibaya zaidi ni kutokujua hatma yao

Fikra ya kutokujua walipo, jinsi walivyokufa ni mbaya zaidi kwa sababu kifo - tumelikubali kifo. Tumezoea wanafamilia wetu kufa kwa sababu hicho ndicho kilichokuwa kinatokea tangu vita kuanza
Alghaly Abderasul
Umoja wa Mataifa unakadiria zaidi ya watu 60,000 waliweza kutoroka jiji hilo, huku takribani 150,000 wakisalia ndani ya jiji. Fatima Abdulrahim aliondoka Al-Fasher pamoja na wajukuu wake siku chache kabla ya jiji hilo kutekwa, wakitoroka hadi mjini Tawila ulio karibu. Anasema waliweza kuepuka ghasia mbaya zaidi za R-S-F lakini waliporwa walipokuwa wakikimbia.

Walipiga wavulana na kuchukua kila kitu tulichokuwa nacho; walituacha bila kitu. Baada ya kuwasili hapa, tuliGUNDUA kwamba wasichana katika kundi lililokuja baada yetu walibakwa, lakini wasichana wetu walifanikiwa kutoroka
Fatima Abdulrahim
 Moja ya mashirika ya kibinadamu yanayosaidia wale waliohamishwa hadi Tawila ni Plan International. Hayley Cull, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Plan International Australia, anasema kwamba ripoti ambazo timu zao zinapokea ni mbaya sana.

 
Wanawasili wakizungumza kuhusu miili ya wafu kando ya barabara kwenye safari. Wanazungumzia watu wanaouawa na kunyongwa, raia wakilengwa kiholela. Watu wanawasili wakiwa wamedhoofika sana kwa njaa. Tunapokea madai ya unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa wanawake wengi, wasichana na watoto.
Hayley Cull
Mlipuko huu wa ukatili unafuatia kuzingirwa kwa muda wa miezi 18 kwa Al-Fasher, ambapo Mtandao wa Madaktari wa Sudan unasema takriban watu elfu kumi na wanne waliaga dunia kutokana na mabomu, njaa na mauaji ya kiholela.

Mnamo mwezi wa Agosti, SBS ilizungumza na Mohamed Douda ndani ya Al-Fasher, ambapo alielezea hali za njaa ambazo raia walikuwa wakikumbana nazo. Alikuwa akisaidia mara kwa mara katika kuripoti mashambulizi kwenye Al-Fasher, na kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam.

Wakati wa mazungumzo haya, alionyesha mara kadhaa kuwa anaamini yeye pamoja na wengi wengine wangeuawa ikiwa wanamgambo wa RSF wangeshika udhibiti wa mji huo.

Ikiwa watachukua udhibiti wa al-Fashir, kutakuwa na mauaji, ubakaji, na utekaji nyara. Kwanza kabisa, watawaua viongozi. Watanikamata, kunitia gerezani na - kama hawataniua - mtahitaji pesa kunikomboa.
Mohammed Douda
 

Marafiki na familia ya Mohamed Douda wamekiri sasa kuwa, wakati R-S-F walivamia mji wa Al-Fasher, aliuawa.

R-S-F walishutumiwa kwa mauaji ya kimbari na serikali ya Marekani na makundi kadhaa ya haki za binadamu mwezi Januari, huku mashambulizi haya ya karibuni yakiibua wasiwasi wa kimataifa wa kampeni ya kutakasa kabila dhidi ya makundi ya asili ya Kiafrika ya Darfur.

Kikosi cha RSF wamekana madai yote ya mauaji ya kimbari. Katika kujibu wasiwasi huu wa karibuni, kiongozi wa kundi hilo, Mohamed Hamdan Dagalo, amedai kuwa ukiukaji wowote wa sheria za kibinadamu za kimataifa huko Al-Fasher ulikuwa tukio la pekee, na aliahidi kuadhibu wanamgambo wowote waliovunja sheria.

 
Kuna ukiukwaji uliofanyika huko Al-Fasher. Kutoka hapa, tunatangaza kuundwa kwa kamati ya uchunguzi. Kamati ya uchunguzi itaanza mara moja kutafiti na kuwawajibisha askari yeyote au afisa yeyote ambaye alifanya kosa au kuvuka mipaka dhidi ya mtu yeyote. Watakamatwa mara moja na matokeo yatatangazwa mara moja na hadharani mbele yenu nyote
Mohamed Dagado

Abdullah Ali, Mwanachama Mtendaji wa Mtandao wa Utetezi wa Wasudan wa Australia, anasema madai haya yanapingana na ushahidi wote uliopo.

Madai haya yanakinzana na ripoti z kutoka kwa mashirika ya kibinadamu na, bila shaka, mashahidi. Vurugu katika Al-Fasher zinafanana na matendo ya RSF kwingineko kama huko Al Jazeera, kabla huko Khartoum, kila mahali ambapo RSF imewahi kuwa
Abdullah Ali
 

R-S-F iliundwa kutokana na mkusanyiko wa wanamgambo wa Kiarabu wanaojulikana kama Janjaweed ambao, mwanzoni mwa miaka ya 2000, walisaidia serikali kukandamiza uasi kutoka kwa makundi yasiyo ya Kiarabu huko Darfur.

U-N inakadiria kuwa watu wapatao laki tatu waliuawa, na viongozi wa kampeni hiyo wanatafutwa bado na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ,kwa mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu. Nathaniel Raymond, kutoka Maabara ya Yale ya Kibinadamu, anasema kampeni hii ya vurugu si jambo jipya.

Hili ni nini? Je, huu ni mauaji ya kimbari? Ndio, lakini si tu mauaji ya kimbari. Hii ni vita vya mwisho kwa kukamilisha mauaji ya kimbari ya Darfur ,ambayo yalianza miaka 20 iliyopita. Kiwango cha mauaji, vurugu kali ambapo kuna uwezekano wa kuonekana mabwawa ya damu kutoka angani pamoja na kasi ya vurugu, ni tofauti na chochote nilichowahi kuona katika kazi yangu. Na nimefanya kazi Syria, pia nimefanya kazi Afghanistan. Hakuna hata moja inayokaribia kiwango tunachozungumzia.
Nathaniel Raymond

Baada ya uvamizi wa Al-Fasher, serikali ya Marekani inasema wanafanya kazi pamoja na Jeshi la Sudan na kikosi cha RSF , ili kuhakikisha usitishaji wa mapigano ya kibinadamu nchini Sudan.

Mshauri Mkuu wa Marekani wa Masuala ya Kiarabu na Kiafrika, Massad Boulos, anasema Marekani imeazimia kuona mwisho wa umwagaji damu.

Kilichotokea Al-Fasher katika siku kumi zilizopita ni cha kusikitisha mno. Ukatili ambao tumeuona, bila shaka, haukubaliki kabisa. Tumekuwa tukijitahidi kwa siku karibu kumi zilizopita , ili kumalizia maelezo ya makubaliano haya ya kibinadamu pamoja na pande zote mbili, tukitumaini kumalizia maelezo na tunatumaini kuwa na kitu chanya cha kutangaza hivi karibuni. Lakini hatuwezi kusema zaidi ya hapo kwa sababu iko katika mchakato wa kujadiliwa.
Massad Buolos
 

  Lakini kwa sasa, Algaly Abdelrasoul na Duha Mohammed wanalazimika kukaa na kusubiri usiku kucha bila usingizi kwa habari za familia zao nyumbani.

Ni jambo la kusikitisha na ni vigumu sana sana kushughulikia." "Hisia za hatia kwa waliobaki hai zimekuwa, si mimi tu, zimekuwa zikiwakumba kila mtu wa Sudan niliyewajua au kushirikiana nao - hata zaidi sasa. Mnahisi hatia kwa sababu mlibaki hai, mlitoka huko, mko salama, mnayo nyumba, mna chakula, mna pesa. Imekuwa ngumu sana kushughulikia hatia hiyo
Algaly Abderasul


Share
Follow SBS Swahili

Download our apps
SBS Audio
SBS On Demand

Listen to our podcasts
Independent news and stories connecting you to life in Australia and Swahili-speaking Australians.
Ease into the English language and Australian culture. We make learning English convenient, fun and practical.
Get the latest with our exclusive in-language podcasts on your favourite podcast apps.

Watch on SBS
SBS World News

SBS World News

Take a global view with Australia's most comprehensive world news service