Chama cha Greens kime elezea wasiwasi kuhusu ukosefu wa upatikanaji wa huduma za afya ya akili kwa bei nafuu, baada ya tangazo kuwa zahanati nyingi zaidi zitafungwa kote nchini Australia. Mtoaji binafsi wa huduma yaki saikoloji, Ramsay Health Care, imesema itafunga zahanati 17 kati ya 20 zaki saikolojia inazo endesha kote nchini kufikia mwisho wa Agosti.
Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) imesema watu sitini na watano waliuawa wakati wa maandamano ya hivi karibuni yaliogeuka na kuwa vurugu nchini Kenya wakati polisi wakitumia nguvu kupita kiasi. Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo jana Alhamisi imebaini ukiukaji mkubwa wa viwango vya kikatiba vya uendeshaji wa polisi ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi, ukosefu wa weledi, na kushindwa kulinda usalama wa umma na haki za raia.
Aliyekuwa waziri wa sheria nchini DRC, Constant Mutamba, Jumatano ya wiki hii alikana mashtaka dhidi yake wakati wa ufunguzi wa vikao vya kesi yake kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma, ikiwa ni pamoja na fidia kwa wahanga wa vita mashariki mwa nchi hiyo. Baada ya kupata umaarufu kitaifa kutokana na misimamo mikali, ikiwa ni pamoja na kutaka watu walionaswa wakitumia pesa za walipa kodi kuuawa, Mutamba alijiuzulu kama waziri Juni 18 kufuatia uchunguzi ulioanzishwa dhidi yake. Katika utetezi wake Mutamba anasema yeye ndiye mwathirika wa "njama ya kisiasa" ya kumzuia kupambana na ufisadi nchini DRC.