Maafisa wa jeshi la polisi wana mamlaka mbalimbali ya kiutendaji ambayo wanaweza kuyatumia chini ya sheria, ikiwa ni pamoja na kuuliza maswali, kutoa maelekezo ya 'kutoka ulipo' na kufanya upekuzi. Haya ndiyo unayohitaji kujua kuhusu haki na wajibu wako wa msingi katika mwingiliano wa polisi.
Mambo Muhimu
- Mamlaka ya polisi yanaweza kutofautiana katika majimbo na wilaya.
- Kuto tii agizo lakufanya kipimo cha kupumua/kupuliza ni kosa
- Huenda ukahitajika kisheria kutoa maelezo ya utambulisho lakini ukachagua kutojibu maswali zaidi.
- Tafuta ushauri wa kisheria ikiwa una wasiwasi kuhusu mwingiliano wa polisi.
- Polisi wanaweza tumia nguvu dhidi yangu wakati gani?
- Haki na wajibu wangu wa msingi ni upi ninapofikiwa na polisi?
- Maagizo yakuondoka ulipo ni nini?
- Polisi wanaweza omba kitambulisho changu wakati gani?
- Je naweza rekodi polisi?
- Itakuwaje kama nina wasiwasi kuhusu mwingiliano na polisi?
Je, unajua haki zako za msingi ukisimamishwa na polisi nchini Australia?
Kulingana na Samantha Lee, msaidizi wa wakili mkuu katika Kituo cha Kisheria cha Redfern, watu wengi, wawe wamezaliwa Australia au kama ni wageni nchini humu, hawajui mipaka ya mamlaka ya polisi.
Polisi wanaweza tumia nguvu dhidi yangu wakati gani?
Dhana potofu ya kawaida kuhusu mamlaka ya polisi inahusu matumizi ya nguvu.
"Ni muhimu kwa watu kujua kwamba kwa sababu tu wao ni maafisa wa polisi, hawana haki ya kutumia nguvu."
Wanaweza tumia nguvu katika hali fulani, lakini tu kama ni lazima katika hali hizo.Samantha Lee
Matumizi ya nguvu 'inayofaa' kama suluhisho la mwisho lazima yawe sawa; si zaidi ya kile kinachohitajika.
Kuna sheria zinazofanana kote nchini kuhusu wakati ambapo polisi wanaweza kutumia nguvu kihalali.
Hata hivyo, kila mamlaka nchini Australia ina sheria yake inayosimamia mamlaka ya polisi.
"Kwa hivyo, unahitaji kuangalia sheria za jimbo na wilaya yako."

Haki na wajibu wangu wa msingi ni upi ninapofikiwa na polisi?
Ingawa katika baadhi ya visa unahitajika kisheria kutoa maelezo ya utambulisho, hakuna wajibu wa jumla wa kubeba kitambulisho nchini Australia.
Hata hivyo, katika majimbo na maeneo mengi ya Australia, lazima ubebe leseni halali ya udereva wakati wowote unapoendesha gari. Katika baadhi ya maeneo, unaweza kuruhusiwa hadi siku mbili kuwasilisha leseni yako ya udereva katika kituo cha polisi ikiwa huwezi kuiwasilisha inapohitajika.
Ikiwa polisi watauliza jina lako na anwani yako, wanahitaji kukuambia sababu za kukusimamisha na kutafuta kitambulisho chako.
Katika mwingiliano wowote wa polisi, Bi. Lee anasema inashauriwa kumwomba afisa awashe kamera yao iliyovaliwa kwenye sare yao.
"Na video inapowashwa, waulize kwa nini umesimamishwa."
Misamaha inaweza tumika, lakini kwa ujumla hulazimiki kisheria kujibu maswali zaidi ya utambulisho. Klaire Coles, ni mkurugenzi wa sheria katika Kituo cha Sheria cha Caxton cha Brisbane anaelezea.
"Watu wanapaswa kuwa na ushirikiano iwezekanavyo […] wanaweza kuwa na adabu na kuzingatia kile kinachoombwa, lakini pia wasitoe taarifa zaidi ya ile polisi wanahitaji ili kufanya kazi yao.
"Wana haki ya kukaa kimya na kutosema chochote ambacho kinaweza kuwatia hatiani kwa kosa la jinai," Bi. Coles anasema.

Maagizo yakuondoka ulipo nini?
Polisi wanaweza toa maagizo ya kisheria papo hapo, wakikuomba uondoke kwenye nafasi ya umma na ukae mbali kwa muda mfupi, kwa kawaida hadi saa 24.
Sheria katika kila mamlaka hutaja sababu zinazowaruhusu polisi kutumia mamlaka ya kuondoka.
Zinajumuisha visa ambapo wana imani nzuri kwamba unazuia trafiki, unamnyanyasa mtu mwingine au unaleta hatari ya usalama.
Ni haki yako kuuliza kwa nini wanatoa amri ya kuondoka.
"Ukiombwa kuondoka mahali fulani au kuhama kutoka eneo fulani, kuelewa ni kwa nini, kwa muda gani, mahali unapopaswa kwenda, kile ambacho polisi wanakuomba ufanye, ni muhimu sana," Bi. Coles anasema.
Polisi wanaweza omba kitambulisho changu wakati gani?
Polisi wanahitaji sababu halali ya kuomba kitambulisho chako katika hali zilizoainishwa katika sheria za jimbo na wilaya.
Marlene Dixon, ni mkurugenzi wa sheria katika Inner Melbourne Community Legal, anaelezea hali kuu:
- Kama polisi wana amini mtu amefanya au yuko karibu kufanya kosa
- Kama mtu anaendesha gari, boti au gari lingine
- Kama wako katika usafiri wa umma
- Kama wako katika sehemu inayo toa huduma ya pombe
- Kama polisi wana amini wana taarifa ambazo zinaweza saidia kuchunguza uhalifu mkubwa

Kote nchini Australia, madereva wanatakiwa kisheria kusimama ikiwa polisi watawasha king'ora chao au kuna kipimo cha kupuliza cha nasibu kando ya barabara.
"Polisi wana mamlaka makubwa linapokuja suala la kuwasimamisha watu na kuwaomba wafanye kipimo cha kupuliza."
Unahitaji tii agizo la kufanya kipimo cha kupuliza. Usipofanya hivyo, unaweza kushtakiwa kwa kosa.Marlene Dixon
Je naweza rekodi polisi?
Kurekodi video ya mwingiliano wa polisi katika eneo la umma kunaruhusiwa kote nchini Australia, mradi tu mtu anayerekodi filamu haingiliani na maafisa.
"Watu wanaweza kurekodi video ya polisi, lakini wanahitaji tu kuhakikisha kuwa inafanywa kwa mbali na kwa heshima, ili isiwazuie polisi katika majukumu yao," Bi Dixon anasema.
Polisi hawawezi kisheria kuchukua kifaa cha mtu anayerekodi kwa sababu anawarekodi.
"Wanahitaji kutafuta kifaa hicho kupitia mifumo rasmi ikiwa watafanya hivyo."

Itakuwaje kama nina wasiwasi kuhusu mwingiliano na polisi?
Polisi wameagizwa kufuata sheria na taratibu.
"Ikiwa unafikiri polisi wametenda kinyume cha sheria, kwa ukali tu au wamefanya kashfa ya ubaguzi wa rangi, unapaswa kuandika mara moja au utakapofika nyumbani kilichotokea," Bi. Lee kutoka Kituo cha Sheria cha Redfern anasema.
Unapaswa pia:
- Kuhifadhi video hiyo kama ulirekodi mwingiliano huo
- Pata ripoti ya daktari na picha kama ulipata majeraha yoyote
- Tafuta ushauri wakisheria.
* Taarifa hii ni ya jumla na haitoi maelezo yote yanayowezekana na sheria tofauti katika maeneo mbalimbali. Unapaswa kutafuta ushauri wa kisheria kwa taarifa mahususi kwa hali yako.
Jisajili au fuata podikasti ya Australia Yafafanuliwa kwa taarifa na vidokezo muhimu zaidi kuhusu kuanza maisha yako mapya nchini Australia.
Je unaswali au pendekezo la mada? Tuma barua pepe australiaexplained@sbs.com.au






