Jimbo la Victoria lina zindua kampeni kuwasaidia watu ambao wako nyumbani na dalili ndogo za UVIKO-19. Sehemu ya kampeni hiyo itawakumbusha watu kuwa, simu kwa 000 ni kwa hali ya dharura, si kwa dalili ndogo. Kampeni hiyo imejiri wakati Victoria imeripoti idadi ya vifo 29 vya ziada vya UVIKO, maambukizi 14,836 mapya na watu 1,057 wanatibiwa hospitalini wakati watu 119 wanahudumiwa katika kitengo cha wagonjwa mahtuti hospitalini.
Muungano wa kisiasa wa One Kenya Alliance nchini Kenya uliowaleta pamoja wanasiasa wa muda mrefu, ambao kwa mwongo mmoja sasa wamekuwa katika upinzani nchini humo, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula na Gideon Moi, uko katika hatari ya kusambaratika baada ya Musalia Mudavadi kutangaza ushirikiano na makamu wa rais wa nchi hiyo William Ruto. Musalia Mudavadi, Makamu wa Rais wa zamani anaandamwa na madai ya usaliti kutoka kwa vinara wenzake, kwa kukaribisha usuhuba wa kisiasa na William Ruto ambaye wamekuwa wakimshambulia kwa maneno.
Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema, inawaweka tayari wanajeshi wa ziada na kupeleka meli zaidi pamoja na ndege za kivita Ulaya Mashariki. Hatua hiyo imekuja wakati Ireland ikitahadharisha kwamba luteka mpya za kijeshi za Urusi nje ya pwani yake hazikubaliki kutokana na mivutano iliyopo kuhusu suala la madai kwamba rais Vladmir Putin analenga kuishambulia Ukraine.