Kampuni ya kutengeneza dawa ya Moderna imesema kwamba inataka idhini ya dharura kwa ajili ya kutumia chanjo yake dhidi ya virusi vya Corona hapa nchini Marekani na Ulaya. Hii ni baada ya chanjo hiyo kuonyesha ufanisi wa asilimia 94.
Kiongozi wa jimbo la kaskazini la Ethiopia linaloshuhudia mapigano la Tigray Debretsion Gebremichael amemwambia Waziri Mkuu Abiy Ahmed aache ukorofi na aondoe wanajeshi wake mara moja. Amemtaka Abiy kuondoa wanajeshi hao katika jimbo hilo ambalo Gebremichael anadai linaendelea kushuhudia mapigano makali licha ya serikali kutangaza ushindi siku mbili zilizopita.
Kenya imesema kwamba haijapokea ilani yoyote inayoitaka kumrudisha nyumbani balozi wake nchini Somalia kufuatia madai ya kuingilia masuala ya ndani na yale ya kisiasa ya taifa hilo. Nairobi pia ilipinga shutuma hizo ikizitaja kuwa zisizo na Ushahidi wowote. Mogadishu pia iliagiza balozi wa Kenya nchini Somalia Lucas Tumbo kurudi Nairobi.