Baraza la Seneti la Marekani, Jumamosi lilipiga kura na kumpata bila hatia rais wa zamani Donald Trump aliyekabiliwa na shtaka la kuchochea ghasia za tarehe 6 Januari, 2021. Katika kesi hiyo iliyochukua takriban siku tano, waendesha mashtaka walisisitiza kwamba Trump alihusika moja kwa moja katika kuchochea ghasia hizo zilizopelekea maafa, majeraha na uharibifu mkubwa wa mali.
Rais Sahle Work Zewde wa Ethiopia akamilisha ziara ya siku mbili nchini Burundi ambako alikuwa na mazungumzo na Rais Everiste Ndayishimiye juu ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao mbili. Mazungumzo yao yaligusia ushirikiano wa kikanda na viongozi hao wameongelea pia suala la kuboresha matumizi ya maji ya mto wa Nile ili kuepusha mizozo inayojiri mara kwa mara kwenye mto huo.
Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa Somalia ameitisha mkutano na viongozi wa majimbo matano ya nchi yake ili kujadili mzozo ulojitokeza wa kutayarisha uchaguzi wa rais na bunge baada ya muda wa muhula wake wa kwanza kumalizika Jumatatu usiku.Taarifa hiyo imetolewa siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwataka viongozi wa Somalia kurudi mara moja kwenye mazungumzo ya kutayarisha uchaguzi, wakati taifa hilo likizidi kukabiliwa na mashambulio kutoka kundi la Al Shabab.