Idara ya serikali ya Marekani inayoratibu shughuli ya kubadilishana madaraka, imempatia rais mteule Joe Biden idhini ya kuendelea na mchakato wa kukabidhiana madaraka huku Trump naye akionekana kukubali kutoa ushirikiano. Hata hivyo Trump amekataa kukubali matokeo hayo akisema ataendelea kupambana mahakamani.
Aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo katika taifa la jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo ubakaji wa watu wengi. Mahakama ya kijeshi ilimpata Ntabo Ntaberi na hatia ya muaji, ubakaji, utumwa wa kingono na kuwasajili watoto walio chini ya miaka 15 katika jeshi lake.
Vikosi vya jimbo la kaskazini mwa Ethiopia Tigray, vijulikanavyo kama Ukombozi wa Watigray-TPLF, vimeharibu uwanja wa ndege katika mji wa zamani wa Axum. Shirika la habari linaloshirikiana na serikali limeripoti hayo leo baada ya vikosi vya serikali ya shirikisho vinavyoendelea kuukaribia mji mkuu wa Tigray Mekelle kuwapa muda wa saa 72 kusalimu amri.