Serikali ya shirikisho imesimamisha safari zote za ndege za abiria kutoka India zinazo kuja Australia, hadi angalau tarehe 15 ya Mei 2021. Vizuizi vimewekwa pia kwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dubai, Singapore na Kuala Lumpur. Waziri Mkuu Scott Morrison amesema idara ya maswala yakigeni na biashara DFAT, itatuma mifuko ya misaada India.
Waziri mkuu Roble anasema alisikitishwa na ghasia za usiku wa jumapili katika mji mkuu, Mogadishu, kati ya vyombo vya usalama vya serikali na vikosi vya upinzani. Aliongeza kuwa mazungumzo na kuelewana ndio njia pekee za kutatua mkwamo wao. Wapiganaji wa upinzani wakiwa na silaha kali walijiweka katika hali ya utayari, katika sehemu mbalimbali za mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, Jumatatu.
Jenerali wa zamani wa jeshi la Burundi Cyrille Ndayirukiye ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha maisha jela kwa shutma za kujaribu kuuangusha utawala wa hayati rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amefariki Jumamosi. Ndayirukiye aliyehukumiwa tarehe 13 Mei 2015, aliaga dunia akiwa katika gereza la mkoa wa Gitega, katikati mwa Burundi, vyanzo vya habari nchini humo vimesema.