Mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya leo yameidhinisha utekekelezaji wa makubaliano ya kibiashara na Uingereza kuanzia Januari Mosi. Msemaji wa urais wa Ujerumani wa Umoja wa Ulaya, Sebastian Fischer, amesema mabalozi kutoka mataifa hayo wameidhinisha makubaliano hayo mjini Brussels leo.
Vitengo muhimu vya usalama vimefanyiwa uharibifu mkubwa chini ya utawala wa rais Donald Trump , rais mteule wa Marekani Joe Biden amesema. Kwa wiki kadhaa baada ya uchaguzi huo wa Novemba 3, Bwana Biden alizuiliwa kupata habari muhimu za kijasusi , ikiwa ni muhimu na utaratibu wa kawaida katika mchakato wa kumkabidhi rais mteule mamalaka.
Mlinzi wa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, amefariki duniani katika mazingira tatanishi Jumapili. Ripoti za vyombo vya habari Uganda vinakariri mashahidi wakisema kwamba Francis Kalibala, aligongwa na gari la jeshi la Uganda UPDF wakati msafara wa Bobi Wine ulikuwa unarudi Kampala kutoka Masaka katika kampeni. Lakini msemaji wa jeshi la Uganda Brig. Flavia Byekwaso amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba Francis alianguka kutoka kwa gari lililokuwa linaendeshwa kwa mwendo wa kasi.