Idadi inayoongezeka ya wajumbe wa Republican wanaungana na juhudi za Rais Donald Trump za kuubatilisha uchaguzi, wakiapa kuyakataa matokeo ya uchaguzi huo wakati Bunge litakapoandaa kikao wiki ijayo cha kuhesabu kura za wajumbe maalum maarufu kama Electoral College na kuidhinisha ushindi wa Rais mteule Joe Biden.
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi ameomba maseneta waliokaribu naye kuunda kundi la maseneta na wabunge wanaoweza kumsaidia kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri linalotawaliwa na watu wanaomuunga mkono aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila. Tshisekedi alivunja mkataba wa kugawana madaraka na Kabila, mnamo mwezi Desemba.
Watu wenye silaha wamewauwa raia 56 na kujeruhi wengine 20 katika shambulizi baya kabisa nchini Niger lililotokea siku ya Jumamosi. Taarifa iliyotolewa na waziri wa mambo ya ndani wa Niger Alkache Alhada imesema shambulizi hilo limetokea kwenye vijiji vya Tchomb-Bangou na Zaroumdareye vilivyo jirani na mpaka na kati ya nchi hiyo na Mali.