Australia ni nchi kubwa na yenye mambo mengi ya kuvutia ya kugundua, lakini kuendesha gari katika maeneo ya vijijini na yaliyo mbali kunaweza kuhusisha hali ambazo huenda usikutane nazo mijini. Kujua nini cha kutarajia na jinsi ya kujiandaa kunaweza kusaidia kusafiri kwa usalama zaidi na kwa kujiamini.
Key Points
- Before you leave, make sure your vehicle is roadworthy and you have appropriate safety equipment and supplies.
- Road and weather conditions can change quickly. Check official information before and during your journey and never drive through floodwater.
- Drive safely to the conditions, take regular breaks and only overtake when it is safe and legal to do so.
Nawezaje jiandaa kwa safari ya barabarani?
Nawezaje endesha gari kwa usalama katika barabara za vijijini na katika maeneo ya mbali nchini?
Nawezaje pata taarifa kuhusu barabara na hali ya hewa?
Nawezaje tumia barabara na sehemu zamapumziko kwa usalama?
Nawezaje jiandaa kwa safari ya barabarani?
Maandalizi ni muhimu kama unapanga kuanza safari ya barabarani kuelekea maeneo ya vijijini na yaliyo mbali nchini Australia.
Kabla ya kuondoka, chunguza hali ya barabara na ya hewa kwa wakati huo, na uhakikishe kuwa gari lako limefanyiwa matengenezo na liko tayari kwa safari, kama anavyoeleza Rhys Heron, kutoka Royal Automobile Club of WA (RAC WA).
"Kagua matairi, taa na breki za gari lako kabla ya kuanza safari; gari lililotunzwa vizuri ni muhimu ili kudumisha usalama barabarani. Ikiwa unavuta trela au 'caravan', kagua matairi yake pia, na uhakikishe kuwa uzito umesawazishwa ipasavyo."
"Hata kama umewahi kufanya safari hiyo hapo awali, huenda hali ya barabara imebadilika tangu safari yako ya mwisho; na hakuna kitu kibaya zaidi kuliko kupotea ukiwa mbali na nyumbani baada ya kuendesha gari katika mazingira yenye mkazo mkubwa—hiyo si njia bora ya kuanza likizo yako," anasema Bw. Heron.

Chukua vifaa na zana za usalama zinazofaa kwa safari hiyo, anaongeza Kylee Petersen kutoka Idara ya Usafiri na Barabara Kuu ya Queensland.
"Hakikisha una chakula cha kutosha, maji, vifaa vya huduma ya kwanza, akiba ya mafuta, vifaa vya kusaidia gari likikwama, na angalau matairi mawili ya ziada ikiwa unasafiri kwenye barabara zisizo na lami," anasema Bi. Petersen.
"Maeneo ya vijijini na ya mbali nchini Australia ni mapana sana, na mtandao wa simu unaendelea kuboreka taratibu kufikia kiwango kinachohitajika; hata hivyo, ikiwa unaweza kubeba simu ya satelaiti au kifaa cha redio cha kutuma ishara ya dharura (EPIRB), ni jambo zuri sana—lakini pia hakikisha unajua jinsi ya kuvitumia ipasavyo."
Kabla ya kuondoka, mjulishe mtu kuhusu unakoenda, njia unayopanga kutumia, na wakati unaotarajia kufika.
Wajulishe familia na jamaa zako unachofanya, unakoenda, na kwamba unasafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine leo na safari hiyo itachukua muda fulani.Kylee Petersen
"Pia, zingatia kuwapa taarifa mamlaka za eneo husika—kama vile halmashauri au polisi—ikiwa unatumia njia za pembeni au zisizo na watu wengi; hili ni ili, iwapo jambo baya litatokea, watu wajue wapi pa kuanzia kukutafuta."
Nawezaje endesha gari kwa usalama katika vijijini au katika maeneo ya mbali nchini?
Hali ya barabara za vijijini na maeneo ya mbali nchini Australia inaweza kutofautiana, huku kukiwa na umbali mrefu kati ya miji, vituo vya mafuta na huduma nyinginezo. Unaweza pia kukutana na wanyamapori, mifugo inayozurura na mabadiliko ya hali ya hewa.
Usiendeshe gari katika maji ya mafuriko au kuingia katika barabara iliyofungwa kutokana na mafuriko.
Weka usalama barabarani kuwa kipaumbele chako cha juu. Punguza kasi, pumzika mara kwa mara na ubadilishane na dereva mwingine ikiwa inawezekana ili usichoke kupita kiasi wakati wa kuendesha, na jaribu kuepuka kuendesha gari usiku.Rhys Heron
Uchovu ni hatari kubwa katika safari ndefu. Ushauri wa serikali kuhusu usalama barabarani unapendekeza kupumzika angalau kila baada ya saa mbili.
"Ikiwa unahitaji kusimama na kuegesha gari kando ya barabara kwa sababu yoyote ya dharura, jaribu kuchagua eneo lenye sehemu pana kando ya barabara, eneo maalum la kuegesha, au kituo cha kupumzikia. Hata hivyo, si wakati wote maeneo haya yanapatikana; Kwa hivyo, kama hayapo, chagua mahali penye mwonekano mzuri kwenye barabara iliyonyooka—si kwenye kona—na uwashe taa za tahadhari."
Kutumia taa za mbele za chini wakati wa mchana kunaweza kufanya gari lako lionekane zaidi kwa watumiaji wengine wa barabara. Wakati wa usiku, kumbuka kupunguza mwanga wa taa inapobidi, ikiwemo unapokaribia gari lingine.
Pita gari lingine tu pale ambapo ni halali na una nafasi pamoja na uwezo wa kuona vizuri ili kufanya hivyo kwa usalama.
Unaweza pia kukutana na misafara ya malori (inayojulikana kama 'road trains'), ambayo ni magari mazito yanayoundwa na lori kuu linalovuta trela mbili au zaidi.
Ben Sutherland ni Rais wa Chama cha Usafirishaji wa Mifugo na Vijijini cha Magharibi Australia, naye anaeleza kuwa kuipita misafara hiyo ya malori kunahitaji umakini na ujuzi.
"Dumisha umbali unaofaa na salama nyuma ya lori... Unapopita, hakikisha ni salama na una nafasi ya angalau kilomita moja ya kufanya hivyo; huenda ukahitaji kuona mbele kwa umbali wa kilomita mbili hivi," anasema Bw. Sutherland.
"Pia, ikiwa msafara wa malori unataka kukupita—kama vile sisi tunavyopita magari yanayo enda polepole—lipe lori hilo nafasi na upunguze kasi kidogo ili liweze kuendelea na safari yake likikupita."
Bw. Heron anasisitiza kuwa inaweza kuwa hatari sana kuipita misafara mikubwa ya malori, hasa ikiwa unavuta gari la burudani (caravan) au trela.
"Malori yanaweza kwenda kwa kasi ya hadi kilomita 100 kwa saa, hivyo muda unaohitajika kuipita misafara hiyo mikubwa ya malori ni mrefu—hadi sekunde 30—na unapokuwa unaendesha, kutumia sekunde 30 ukiwa upande usio sahihi wa barabara ni hatari sana. Kwa hivyo, jambo bora zaidi la kufanya ni kusubiri fursa ya njia maalum ya kupita magari mengine badala ya kuchukua hatari hiyo," anasema Bw. Heron.

Nawezaje endelea kupata taarifa kuhusu barabara na hali ya hewa?
Hali ya barabara inaweza kubadilika wakati wa safari yako, kwa hivyo angalia kufungwa kwa barabara na onyo za hali ya hewa na usitegemee tu urambazaji mtandaoni, kama Bi. Petersen anavyoelezea.
"Beba ramani ya karatasi au urambazaji nje ya mtandao kama nakala rudufu... kwani programu hazionyeshi hali ya barabara iliyosasishwa kila wakati... Na kadri unavyozidi kuwa vijijini na katika maeneo ya mbali, kwa kuwa na ufikiaji mdogo wa simu, programu hizi hazijasasishwa kila wakati haraka iwezekanavyo." anasema.
Vyanzo vya ndani vinaweza pia kukusaidia kuelewa hali ya sasa.
Ni muhimu kuangalia taarifa rasmi za barabara kwa ajili ya jimbo au eneo unalopitia.
Unaweza pia kuangalia utabiri na maonyo kutoka kwa Ofisi ya Hali ya Hewa, pamoja na taarifa rasmi za dharura kwa ajili ya maeneo unayopitia.

Nawezaje tumia barabara na sehemu zamapumziko kwa usalama?
Kuwajali wengine kunahusu pia maeneo unako simama wakati wa safari yako.
"Taka zozote unazozalisha wakati wa safari, hakikisha unaziweka kwenye pipa la taka, na kama hakuna pipa, ondoka nazo. Unapotumia vyoo vya umma, viweke katika hali ya usafi..." anasema Bw. Heron.
Baadhi ya maeneo ya kupumzikia na maeneo ya kuegesha magari yametengwa mahususi kwa ajili ya magari makubwa, ambayo madereva wake wanapaswa kuchukua mapumziko kama sheria inavyoelekeza.
Australia ina mandhari na maeneo ya kuvutia sana ya kutembelea na kufurahia; hivyo, kama Bi. Petersen anavyotukumbusha, kuwa dereva mvumilivu na mwenye adabu kutahakikisha kila mtu barabarani anapata uzoefu mzuri.
“Hali ya kukata tamaa au kuudhika kwa dereva inaweza kusababisha maamuzi mabaya. Kwa hivyo, tafadhali endesha gari kwa kuzingatia hali ya barabara, uwe na subira, uwe macho, na uheshimu barabara pamoja na madereva wengine.”
Jisajili au fuata podikasti ya Australia Yafafanuliwa kwa taarifa na vidokezo muhimu zaidi kuhusu kuanza maisha yako mapya nchini Australia.
Je unaswali au pendekezo la mada?
Tuma barua pepe australiaexplained@sbs.com.au


![[JPG]_How-Australia-Works_Ep0.jpg](https://assets.sbs.com.au/dims4/default/9a0f61e/2147483647/strip/true/crop/3200x1800+0+0/resize/1280x720!/quality/90/?url=https%3A%2F%2Fsbs-au-brightspot.s3.ap-southeast-2.amazonaws.com%2F8f%2F15%2F83a000db458f9fc153fde8cde907%2Fjpg-how-australia-works-ep0.jpg&imwidth=1280)



